Ruka hadi maudhui makuu

Je, Mkristo anapaswa kulikabili vipi janga la ugonjwa?

Open old book

Virusi visivyoweza kudhibitiwa, kama dhoruba kubwa, vinasafiri katika mabara na kuwaambukiza watu walio karibu nasi. Kwa baadhi yetu, vinatunyang’anya kazi zetu na maisha ya watu tuliowapenda. Tunajiona hatuna tumaini mbele ya virusi ambavyo hatuna tiba yake. Tunajihisi kama tunaelea ndani ya mashua ndogo katikati ya dhoruba.

37Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji. 38Yesu alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”
39Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.
40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”
( Marko 4:37-40 )

Ni jambo la kawaida kwetu kujenga matumaini yetu juu ya uzoefu wetu katika ulimwengu huu. Mambo yanapokwenda kama tunavyotarajia, tunatulia na kufurahi. Tatizo dogo linapotujia, tunajaribu kulipuuza na kusonga mbele. Matumaini yetu yanakua pamoja na maendeleo ya viwanda yanayotuletea maisha ya starehe na uvumbuzi wa kisayansi unaoeleza jinsi mambo yanavyofanya kazi na kutengeneza chanjo za magonjwa yote. Hata hivyo, msingi wa imani yetu ni dhaifu sana na huanguka haraka jambo lisilo la kawaida linapotokea. Hebu tuangalie ahadi tuliyopokea kutoka kwa Mungu wetu, Baba.

2Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Bwana Mungu wako:
3 Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na mifugo wako wachanga, yaani ndama wa makundi yako ya ngʼombe, na wana-kondoo wa makundi yako.
5Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.
6 Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.
7 Bwana atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
8 Bwana ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi anayokupa.
11Bwana atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kukupa wewe.
12 Bwana atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote.
13Bwana atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Bwana Mungu wako ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa makini, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini.
( Kumbukumbu 28:2,3,4,5,6,7,8,11,12,13 )

Si jambo la kawaida kwetu kuishi maisha haya tukimtii Mungu na amri zake kikamilifu. Mara tu maisha yetu yanapotoka katika taabu, tunarudia njia zetu mbaya, tena na tena...

15Mara kwa mara nimewatuma kwenu watumishi wangu wote, manabii wakisema, “Geukeni, kila mmoja aiache njia yake mbaya, na kutengeneza matendo yake. Msiifuate wala kuitumikia miungu mingine. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza.
( Yeremia 35:15 )

Tunajiona tukiwa katika hofu na upungufu wa imani. Kizazi baada ya kizazi, kwa maelfu ya miaka, watu wamekuwa wakimwasi Mungu na kupoteza baraka zake. Tumeutikisa upendo kutoka katika msingi wa amri za Mungu, tukabaki na maneno makavu tu, pamoja na utii wa nje na wa kimazoea kwazo. Hayo yote yametufikisha mahali pa hofu, sawasawa na ilivyoahidiwa…

20 Bwana ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, hadi uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye.
22Bwana atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga hadi uangamie.
( Kumbukumbu 28:20,22 )

Hasira ya Mungu kwa kweli inatisha. Lakini kabla hatujaharakisha kumhukumu Baba yetu wa mbinguni kwa kufanya mambo makali kama hayo, hebu tumfikirie daktari anayekata mguu ulioambukizwa ili kumwokoa mtu asife. Ni kawaida kwetu kukazia macho mambo yanayoonekana na kupuuza upendo wa Mungu wetu na hamu yake ya kutuokoa. Mtoto wetu atakumbuka hasira yetu na kofi lenye maumivu mgongoni, lakini atasahau kwa urahisi jinsi lilivyomwokoa asianguke kutoka kwenye jabali hatari. Nasi tunaoona mambo ya duniani tu, hatuoni hata kile ambacho hasira ya Mungu inatuokoa nacho.

Mungu anataka tumtii kwa uaminifu. Anataka tusiogope kile tunachokiona, bali tupate ujasiri kutokana na imani yetu.

18Kwa hivyo hatuangalii yale yanayoonekana, bali yale yasiyoonekana. Kwa maana yale yanayoonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoonekana ni ya milele.
( 2 Wakorintho 4:18 )

Iwe uko katika hatari ya kupoteza maisha yako, au uko katika kilele cha afya yako, kifo huonekana kuwa jambo baya kuliko yote linaloweza kutupata. Lakini je, ni hivyo kweli? Kifo ni jambo la mwisho tunaloliona kwa mwanadamu. Kifo hutufungulia mlango wa yasiyoonekana, wa yasiyojulikana.

Yasiyojulikana katika maisha yetu, au baada yake, hutawaliwa na hofu yetu au na imani yetu. Tunaweza kujizungushia giza la hofu au nuru ya imani. Kama tunavyoona katika maisha haya ya duniani, watu wenye imani hufanikiwa katika kile wanachofanya. Na hakuna sababu ya kutilia shaka kwamba imani itaangaza njia baada ya kifo kwa wale wanaoamini. Njia ya kuelekea maisha bora zaidi kuliko haya ya hapa duniani.

16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
( Yohana 3:16 )

Sasa hivi tuko hai. Nasi tunamshukuru Mungu wetu kwa kila dakika tunayoishi sasa, kwa uwezo wa kuona na kupumua, na wa kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu. Bado tunaweza kuwaona wapendwa wetu na kuwaambia jinsi walivyo na thamani kwetu.

Upendo hushinda hofu na hufunua sisi ni nani hasa, tulioumbwa kwa mfano wa Mungu. Na kwa kupitia kifo cha kimwili na ufufuo, Yesu Kristo alivunja minyororo ya mauti na kutuletea Roho Mtakatifu, msaidizi asiyeonekana ambaye sasa anaweza kuishi ndani yetu.

17Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi, naye anakaa ndani yenu.
( Yohana 14:17 )

Roho tuliyempokea si roho wa hofu, kwa kuwa anatuongoza kwenye uzima wa milele.

7Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
( 2 Timotheo 1:7 )

Kutokana na hili tunaona kwamba, tukihisi hofu, haitokani na Roho ambaye Mungu ametupa. Tukienenda katika giza la hofu, hatujaleta nuru ya imani katika Bwana, Mungu wetu.

12 Kisha Yesu akasema nao tena, akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata, hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
( Yohana 8:12 )

Sasa, ukiwa umesimama katikati ya kitovu cha janga hili, ungechagua nini – hofu au imani? Watu wengine wanapokutazama katika giza la ulimwengu huu wenye hofu, je, wanaweza kuiona nuru yako?

3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,
na maradhi ya kuambukiza ya kuua.
4 Atakufunika kwa manyoya yake,
chini ya mabawa yake utapata kimbilio,
uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.
5 Hutaogopa vitisho vya usiku,
wala mshale urukao mchana,
6wala maradhi ya kuambukiza
yanayonyemelea gizani,
wala tauni iharibuyo adhuhuri.
7Ijapo watu elfu wataangukia kando yako,
kumi elfu mkono wako wa kuume,
lakini haitakukaribia wewe.
( Zaburi 91:3-7 )
9Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe popote utakapoenda.”
( Yoshua 1:9 )

Hakuna kitu kinachotokea bila sababu katika ulimwengu wetu. Je, janga hili litatufundisha nini? Je, tutaweza kweli kuthamini maisha ya mwanadamu? Je, tutaweza kuthamini urafiki wa kweli na kuonyesha shukrani kwa kile tulicho nacho? Je, litakomesha mashindano yasiyo na maana ya kupata picha nzuri zaidi kwenye Instagram na wafuasi wengi zaidi wa video zetu za YouTube? Je, litakomesha vita vya kugombania pesa na mamlaka? Je, litalifanya anga kuwa la buluu tena kwa vizazi vijavyo? Je, hatimaye tutaweza kuondoa pazia machoni petu na kuuona ulimwengu halisi ulioumbwa na Baba yetu?

27Amani nawaachia; amani yangu nawapa. Amani hii ninayowapa si kama ile ulimwengu unatoa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
( Yohana 14:27 )
Neno (NEN)